Wito wa Ombi

1. UTANGULIZI
Anza Entrepreneurs ni shirika lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kujenga uwezo wa wafanyabiashara ambao wanazalisha na kusambaza bidhaa na huduma zinazolenga katika kuboresha maisha ya watanzania, wakati huo huo zikitengeneza nafasi za ajira na kuchangia katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Anza inatoa mafunzo ya mikakati ya biashara, inawaunganisha wafanyabiashara na wadau muhimu, na pia inatoa mitaji rahisi ili kuchochea ukuaji haraka wa biashara na wenye tija katika jamii

Aga Khan Foundation (AKF) ni shirika lisilo la kiserikali, lililo jikita katika kuleta maendeleo ya kijamii ambalo linatafuta suluhisho la muda mrefu kwa matatizo yanayokabili jamii. AKF ina lenga kuwekeza katika uwezo wa binadamu, kupanua fursa, na kuboresha maisha, hasa kwa wanawake na wasichana. AKF hushirikiana na asasi tofauti za kiraia katika kutatua changamoto zinazo kabili jamii zinazotuzunguka. AKF imejikita kutatua changamoto zinazokabili sekta za Elimu, Kilimo, Chakula, maendeleo ya watoto na afya.

Anza kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation chini ya udhamini wa Umoja wa Ulaya tunayo furaha kufungua dirisha la maombi kwa mwaka 2022 kwa programu ya kuongeza uwezo kwa wajasiriamali vijana wanaosaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii ya Tanzania. Ambazo ni:

• Upatikanaji mdogo wa huduma muhimu za kijamii. Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa za kijamii, na idadi kubwa ya watu hawana njia rahisi za upatikanaji wa safi na salama, nishati mbadala, huduma za kifedha, huduma za afya za bei nafuu, elimu bora, na chakula.

• Ukosefu wa ajira. Viwango vya ukosefu wa ajira nchini Tanzania vina ongezeka kila siku. Kila mwaka zaidi ya Watanzania 900,000 huingia katika soko la ajira lakini hakuna ajira za kutosha.

• Mazingira hafifu katika ubunifu. Tanzania ina ukuaji mdogo wa kibiashara kwa sehemu kubwa kutokana na wajasiriamali/wafanyabiashara kutokuwa wabunifu katika kutatua changamoto mbalimbali za wateja wao, na hivyo kudumaza au kuchelewesha ukuaji wa biashara zao kwa kasi, na kuleta tija kwenye jamii husika.

Wajasiriamali wabunifu ni watu muhimu katika kutatua changamoto hizi. Wabunifu wana uwezo wa kutengeneza bidhaa na huduma zinazoweza kutatua changamoto hizi na pia kutengeneza ajira. Hata hivyo wajasiriamali wa hatua za mwanzo mara nyingi hawana mafunzo muhimu, mitandao, na mtaji wa kukuza biashara zao.

2. KUHUSU PROGRAMU
Tunatoa fursa kwa wajasiriamali wabunifu kutoka mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara ambazo zinachangia katika kukabiliana na changamoto kubwa za kijamii katika sekta zifuatazo; Kilimo, Elimu, Afya, Nishati, Maji na Usafi.

Programu imelenga katika kumpatia mjasiriamali
• Mafunzo ya biashara yatakayo wezesha wajasiriamali kupata ujuzi ya namna bora ya uendeshaji wa biashara ili kukuza biashara zao na kuongeza kipato.
• Nyenzo za kuendesha biashara yako.
• Nafasi ya kukuza mtandao wa kibiashara ili kujenga biashara yenye faida na endelevu.
• Mtaji wa kukuza biashara yake

Programu hii itatoka mafunzo ya biashara katika awamu tatu tofauti kama ifuatavyo;
• Warsha (Hackathon): Wajasiriamali 300 watashiriki kwenye warsha ya siku 3 ambapo watapata nafasi ya kuwasilisha/kuelezea biashara zao mbele ya wadau mbalimbali wenye ujuzi na uzoefu kwenye biashara, na biashara 150 zitachaguliwa kuendelea na awamu ya pili ya programu
• Kambi ya mafunzo (Bootcamp): Wajasiriamali 150 waliochaguliwa kutoka kwenye awamu ya kwanza ya programu (hakathoni), watashiriki kwenye kambi ya wiki moja ya mafunzo ya biashara ambapo watapatiwa mafunzo ya msingi ya biashara yanayolenga katika kumsaidia mjasiriamali kutambua, kuelezea tatizo ambalo biashara yake inalenga kulitatua, na kuweka mikakati ya biashara katika kutatua changamoto hizo. Wajasirimali watapata pia nafasi ya kuwasilisha biashara zao, na biashara chache zitachaguliwa kushiriki katika awamu ya tatu ya programu.
• Programu ya kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara (Business Foundation Accelerator): Wajasiriamali 75 watapata nafasi ya kushiriki katika programu kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara kwa miezi sita. Programu hii inajumuisha mfululizo wa warsha zisizopungua 4 kwa siku 3 kila warsha ambazo huwapatia wajasiriamali mafunzo na nyenzo ya kuendeleza biashara zao. Pia wajasiriamali wanapata fursa ya kukutana na washauri na wadau wa sekta husika wanaoweza kuleta tija kwenye biashara zao.

3. VIGEZO VYA USHIRIKI

• Ubunifu. Biashara yenye uvumbuzi(kitu kipya) duniania au kwa Tanzania katika kuchochea upatikanaji wa bidhaa au huduma zinazoboresha maisha au uvumbuzi unaosaidia katika kuboresha mnyororo wa thamani na usambazaji ili kuwafikia watu wenye kipato cha chini na kuboresha maisha yao kupitia huduma na bidhaa zinazotolewa na wajasiriamali.
• Umri. Mmiliki wa biashara awe na umri wa miaka 18 – 35.
• Sekta: Biashara yako iwe imejikita katika sekta ya kilimo, elimu, afya, nishati mbadala, maji na usafi.
• Mauzo: Biashara iwe imeanza shughuli za uendeshaji na inauthibitisho wa mauzo na wateja.
• Hatua ya biashara. Biashara iwe imevuka hatua ya wazo, na iweze kutumia ubunifu kutatua changamoto katika jamii
• Idadi ya wafanyakazi. Tunatarajia biashara kuwa na wafanyakazi kuanzia 1 hadi 3 (ikijumuisha mmiliki kama anafanya kazi katika biashara) wakati wanajiunga na programu yetu. Hii inajumuisha waanzilishi wa biashara pamoja na wafanyakzai wengine.
• Wateja. Kipaumbele chetu kitakuwa biashara ambazo bidhaa au huduma zao zinalenga kumfikia mtumiaji wa mwisho au zinatoa suluhisho la kutatua changamoto kwa mtumiaji wa chini.
• Mchango katika jamii. Je inatatua changamoto zinazokabili jamii inayoizunguka?

4. TAREHE NA MATUKIO
Hakatoni
• Dar es Salaam: 29 Juni – 01Julai, 2022
• Mtwara: 6 – 8 Julai, 2022
• Mwanza: 20 – 22 Julai, 2022

Kwa maelezo zaidi tembelea wavuti wetu www.anzaentrepreneurs.co.tz

5. MWISHO WA MAOMBI
Maombi yatumwe kabla ya tarehe 17 Juni, 2022